Tuesday 27 May 2008

MASUPASTAA KIBAO KUSINDIKIZA TUZO ZA VINARA WA FILAMU
Wasanii nguli wa muziki nchini wamethibitisha kusindikiza utoaji wa Tuzo za Vinara wa filamu Tanzania (Vinara Film Awards 2007-2008) zitakazofanyika ijumaa hii tarehe 30 mei 2008 ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee Hall kuanzia saa mbili usiku.
Habari kutoka ndani ya One Game Promotions wanaoandaa Tuzo hizo, zinasema kuwa, tayari Mzee Yusuf, Profesa Jay, Nakaaya Sumary, Safu ya unenguaji ya Akudo, Matonya na THT Dancers wamethibitisha kutumbuiza siku ya shughuli hiyo kubwa nchini.
Wadadisi wa masuala ya burudani wamesema kwamba Tuzo za Vinara wa Filamu Tanzania ni tukio kubwa la kihistoria hapa nchini na Afrika ya Mashariki. Inatarajiwa Kuwa siku hiyo itakuwa na burudani ya aina yake.
Wiki iliyopita, majaji wa tuzo hizo walitangaza majina matano kwa kila kipengele yaliongia katika hatua ya mwisho ya kuwania tuzo hizo. Washindi kwa kila kipengele wanatarajiwa kukabidhiwa Tuzo hizo siku ya Ijumaa Mei 30 ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee.
Kategori ambazo zinaangaliwa na mashabiki wengi wa sanaa ya maigizo ni zile za waigizaji bora wa kike na kiume wa mwaka 2007-2008 baada ya wasanii nguli wa sanaa hiyo kupigwa chini kwenye uteuzi.
Tuzo ya Muigizaji bora wa kike inawaniwa na Lucy Komba (Diversion of Love), Grace Michael (Malipo ya Usaliti), Halima Yahya (The Stranger), Elizabeth Chijumba (Copy) na Riyama Ally (Fungu la Kukosa).
Kwa upande wa muigizaji bora wa kiume, tuzo inawaniwa na Single Mtambalike (Agano la Urithi), Nurdin Mohammed (Utata), Jacob Steven (Copy), Hajji Adam (Miss Bongo) na Yusuf Mlela (Diversion of Love).
Fainali za Tuzo Vinara wa Filamu zinatarajiwa kufanyika tarehe 30 mwezi huu ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee kuanzia saa mbili usiku. Kiingilio ni Tshs 20,000 kwa viti maalum na Tshs 10, 000 kwa viti vya kawaida.
Watakaofika kwenye ukumbi wategemee mapokezi ya kifahari, kuwekewa zulia jekundu (red carpet) na burudani tosha mithili ya Tuzo za filamu za Oscars za nchini Marekani.
Tuzo hizi zitakazokuwa zinatolewa kila mwaka zimedhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL) kupitia bia ya Ndovu Special Malt ikishirikiana na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Digital Art, Global Publishers, Clouds FM, Regency Park Hotel, KIU Investment na Vayle Springs.
Khadija Halili
Mratibu

No comments: