Thursday 26 July 2007

Noma ya Kiba ni fundisho!


Hivi karibuni, msanii aliyekuja juu kwa kasi katika Bongofleva hasa baada ya kutoka na singo yake `Cinderella` almaarufu kwa jina la Ali Kiba alifikishwa mahakamani akidaiwa shilingi milioni 10 kwa madai ya kuiba mashairi ya wimbo huo kutoka kwa Malaika Kamugisha. Kesi hiyo ya madai nambari 33 ya mwaka 2007 inaendelea kuunguruma katika Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo. Ningependa kuchukua fursa iliyotokana na kufunguliwa kwa kesi ya `Cinderella` kuwaasa wasanii wa Bongofleva kwa ujumla kuogopa kama ukoma vitendo vya wizi wa mashairi na 'beats' kutoka kwa artist wengine.

Ieleweke wazi kuwa duniani kote, mashairi na `beats` ni mali za wasanii waliotoka nazo kwanza hivyo endapo itatokea msanii aliyeibiwa mashairi ama `beats` hizo kuthibitisha mahakamani kuwa yeye ndiye alikuwa wa kwanza kuvitumia, hivyo kuwa ndiye mwenye hakimiliki navyo, sheria inayosimamia nyanja hiyo ipo wazi kwa `mhalifu`. Ni tatizo ambalo lipo ulimwenguni kote hatahivyo, iwe kwa makusudi ama kwa bahati mbaya, na ni tatizo ambalo limewahi kuwakuta wasanii kadhaa nyota wa majuu wakiwemo mfalme wa muziki wa pop (wa zamani?) Michael Jackson na muimbaji nyota wa R n` B sasa Marekani Beyonce Knowles katika siku za karibuni. Kwa hapa nyumbani malalamiko ya wizi, hasa wa mashairi, ni vitu ambavyo vinakaribia kuwa vya kawaida katika Bongofleva ingawa mengi ya malalamiko hayo, tofauti na `Cinderella`, huishia maskani. Kwa hapa nyumbani, pia, malalamiko ya wizi wa `beats` ni mambo yanayokaribia kuanza kuzoeleka kwenye Bongofleva na katika namna inayoonyesha kuwa hatua za haraka zisipochukuliwa Bongofleva itapiku aina anzilishi za muziki nchini, kumekuwepo na madai ya wizi wa viitikio na hata ya wasanii wa nyumbani kukopi kama zilivyo kazi za wasanii wa nje, tofauti ikiwa ni katika tafsri ya lugha tu. Ni vitu ambavyo havipaswi kuendelea kuwepo ndani ya Bongofleva sasa kwasababu mara nyingi njia za mkato katika fani zinasaidia kupatikana kwa maendeleo ya haraka ya msanii, akanunua madini na Baloon. Lakini zina madhara makubwa siku za usoni na hasa kama tupo katika safari ya kujaribu kuiwezesha Bongofleva ishindanishwe pia katika tuzo kama za MTV na nyingine zenye akili. Kimsingi, chanzo cha wasanii wa Bongofleva kuingia katika kashfa za wizi wa mashairi inatokana na ufahamu mdogo uliopo miongoni mwa wasanii wanaoibuka kila kukicha katika fani. Wengi hudhani kuwa msanii ni lazima atunge mwenyewe na aimbe mwenyewe. Ukweli ni kuwa hata wasanii wakubwa wa Marekani kwamfano, hutokea wakatamba katika chati za Top Ten za Billboards na kwingineko mpaka Ulaya kwa wimbo ambao hakutunga yeye. Na singo za `Umbrella` na`Crazy in Love` za Rihanna na Beyonce ni mifano ya karibu. Hivyo tufike mahali wengine waimbe, na wengine watunge na kuwauzia wanaojua kuimba huku wakiwa pia na uwezo wa kulipia gharama kubwa za kurekodi studio.

1 comment:

DERRICK MUSHOBOZI said...

Mkuu hapo sina cha kuongeza nafikiri umemaliza kila kitu nafikiri mwenye masikio atakuwa amesikia hasa hawa wasanii wetu wenye tabia ya kuiba mashairi ya wenzao.